Thursday, April 18, 2013

BREAKING NEWS - ARUSHA: 
"MAELFU WAMZIKA BABU SAMBEKI"

Wakati mazishi ya mfanyabiashara bilionea wa Moshi, Ernest Babu ‘Sambeke’ yakiwa yamepangwa kufanyika keshokutwa, msiba wake umekuwa wa kitajiri kutokana vyakula na vinywaji kumwagwa kwa wingi nyumbani kwa marehemu.

Msiba wa mfanyabiashara huyo uko nyumbani kwake, Njiro – Themi nje kidogo wa Mji wa Arusha ambako habari zinasema mamia ya watu wamekuwa wakifurika kuhani.

Matajiri wa Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha wakiwa na magari ya kifahari wamefurika katika msiba huo na habari zaidi zinasema mamilioni ya shilingi yamechangwa kwa ajili ya kufanikisha mazishi ya bilionea huyo aliyefariki dunia, Jumamosi iliyopita kwenye ajali ya ndege.

Ajali hiyo ilitokana na ndege aina ya MT 7- yenye namba 5H-QTT ambayo alikuwa akiiendesha mwenyewe kuanguka kwenye Uwanja wa Ndege wa Arusha, baada ya bawa lake kugonga mti katika eneo la Magereza linalopakana na uwanja huo.

Alifariki dunia wakati askari magereza waliompa msaada walipokuwa wakimkimbiza hosipitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata kichwani.

Meneja wa Uwanja wa Ndege Arusha, Ester Dede alisema uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea kufanywa na wataalamu wawili wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga kutoka Dar es Salaam.

Magari makubwa yaliyosheheni vyakula na vinywaji yamekuwa yakiingia na kutoka katika makazi ya Sambeke ambako waombelezaji wote wameandaliwa maeneo maalumu ya kuketi yaliyofunikwa na mahema ambako vinywaji na vyakula vinatolewa.

Msemaji wa familia, Dk Richard Masika alisema marehemu atazikwa katika eneo la Karanga mjini Moshi ilipo nyumba yake na kwamba misa itaanza saa 7.00 mchana katika Kanisa Katoliki mjini Moshi na mazishi kufanyika saa 10.00 jioni.

Habari zaidi zilizopatikana zinaeleza kuwa marehemu atazikwa akiwa amevalia sare za marubani kutokana na kupenda kwake kurusha ndege.

Habari zaidi zinasema familia ya marehemu imekuwa ikifuatilia mali alizokuwa nazo marehemu zikiwemo fedha wakati akipatwa na mauti.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alisema, Babu Sambeke alikuwa ni rafiki wa watu wengi, wakiwapo wanasiasa wa vyama vyote.

“Binafsi baada ya kupata taarifa za kufariki kwa Babu Sambeke, niliwapigia baadhi ya wabunge na mawaziri, wote walishtushwa sana na msiba huu,” alisema Nassari.

Babu Sambeke ni mmoja wa wafanyabiashara wa kwanza katika kanda ya Kaskazini kumiliki ndege, na hadi anafariki alikuwa akitumia 
ndege mbili.


Ndege aina ya Cessna  5H-QTT  ikiwa imeanguka eneo la Kisongo,  karibu na Uwanja wa Ndege Arusha  juzi jioni, baada ya kugonga mti wakati ikijiandaa kutua  na kusababisha kifo cha mmiliki wake na aliyekuwa Rubani, Bob Sambeke(katika picha ndogo).


No comments:

Post a Comment