Thursday, September 13, 2012

Filamu ya Kumkashifu Mtume Yasababisha Balaa, Balozi wa Marekani Auliwa

Filamu hiyo iliyotengenezwa na Mmarekani mwenye asili ya Israel, Sam Bacile mwenye umri wa miaka 52 ilitengenezwa California nchini Marekani ikiwashirikisha wasanii mbalimbali.

Filamu hiyo inayokwenda kwa jina la "Innocence of Muslims" imetengenezwa kwa lugha ya kiingereza ikiwa na tafsiri ya maandishi kwa kiarabu.

Filamu hiyo imegharimu dola za Marekani milioni tano kuitengeneza kwa msaada wa mayahudi 100 waliojitolea kuchangishana fedha za kuitengeneza filamu hiyo.

Baadhi ya klipu za filamu hiyo zimewekwa kwenye YouTube zikimuonyesha mtu aliyeigiza kama mtume Muhammad, akifanya mapenzi, akibaka na akiamuru kuuliwa kwa watu.

Muda mwingi katika filamu hiyo, muigizaji huyo aliyejifanya mtume alikuwa akiitwa kwa majina mbalimbali kama mbakaji wa watoto, fisadi na majina mengine mbalimbali.

Mtengezaji na mhakiki wa filamu hiyo ya kuukashifu uislamu aliuita uislamu kuwa ni hatari kama ugonjwa wa kansa.

Kufuatia kutolewa kwa filamu hiyo, waislamu katika sehemu mbalimbali duniani wameonyesha kukerwa na kitendo hicho na kuvamia balozi za Marekani.

Nchini Libya watu wenye silaha walivamia ubalozi wa Marekani mjini Benghazi na kuuchoma moto na kumuua balozi wa Marekani nchini Libya Christopher Stevens pamoja na wafanyakazi watatu wa ubalozi huo.

Balozi huyo wa Marekani aliuliwa baada ya gari lake alilokuwemo kurushiwa kombora ndani ya ubalozi huo.

Mjini Cairo, nchini Misri, waislamu wenye hasira waliuvamia ubalozi wa Marekani na kuuchorachora ukuta wa ubalozi huo na kuishusha bendera ya Marekani na kuichanachana vipande vipande kabla ya kuipandisha bendera ya nyeusi ya uislamu.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton alithibitisha kuuliwa kwa balozi huyo na alilaani shambulizi hilo na kumtaka rais wa Libya, Mohammed el-Megarif aongeza ulinzi kwa raia wa Marekani nchini Libya.

Clinton alielezea hofu yake ya mashambulizi hayo kwenye balozi za Marekani huenda zikasambaa kwenye nchi zingine.
Clinton aliongeza kuwa Marekani inalaani vitendo vyote vya kuchochea uhasama kwa kukashifu dini zingine lakini alisisitiza kuwa kitendo hicho kisitumiwe kama kigezo cha kuanzisha vurugu.

No comments:

Post a Comment