TUNDUMA - MBEYA.MGOMO WA WALIMU,IMEKUWA FURSA KWA VIBAKA KUNUFAIKA.
Kufuatia Mgomo wa walimu ulioanza jana, wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi katika Mji mdogo wa Tunduma,Wilaya ya Momba Mkoani Mbeya waliamua kuandamana ili kudai haki ya kufundishwa katika maandamano ambayo yaliingiliwa na vibaka ambao baadaye walivunja ofisi za Halmashauri ya mji huo na kuiba mali kadhaa kisha kuchoma nyaraka zilizokuwemo.
Hatua hiyo ilijitokeza mapema saa 2 asubuhi wakati wanafunzi wa shule 14 za msingi zilizopo katika halmashauri wa Tunduma,walipojikusanya na kufanya maandamano hadi nyumbani kwa diwani ambapo baada ya kumkosa walielekea kituo cha polisi cha mjini hapa kabla ya kufika ofisi za halmadhauri ya mji.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa, awali wanafunzi hao walikwenda nyumbani kwa Diwani wa kata ya Tunduma mheshimiwa Frank Mwakajoka (CHADEMA) na baada ya kufanya mazungumzo na mke wa diwani huyo ambaye inadaiwa hakuwepo waliandamana hadi kituo cha polisi na kuelekea katika ofisi za halmashauri ya mji ambapo msafara huo uliingiliwa na baadhi ya watu walioendesha uporaji huo.
Mmoja wa shuhuda hao ambaye alijitambulisha kuwa ni Julius Edward, alidai kuwa baada ya wanafunzi hao kufika katika ofisi za polisi walipokelewa na kufanya mazungumzo ambayo maamuzi yake hayakuafikiwa na wanafunzi hao.
Alisema baada ya kutoafiki majibu yaliyotolewa na Polisi wanafunzi hao waelekea kwenye mzunguko wa barabara uliopo karibu na eneo la ofisi za Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) katika mpaka wa Tanzania na Zambia ambako walizuia barabara ili magari yasipite.
Usumbufu huo ulidaiwa kujitokeza kwa muda wa nusu saa, hatua ambayo ilisababisha polisi wa kituo hicho kufika eneo hilo na kulazimika kuwatawanya wanafunzi hao kwa kutumia mabomu mawili ya machozi hali ambayo ilisababisha vibaka kujiingiza na kuaanza uporaji kwa kukimbilia ziliko ofisi za halmashauri ya mji.
Watu hao ambao wameonekana wakivamia ofisi hizo na kuchoma moto baadhi ya mali za halmashauri hiyo huku wakipora kompyuta 5 za ofisi, pikipiki yenye namba STK 6264, kumbukumbu na nyaraka mbalimbali sambamba na kuvunja milango ya ofisi zote, kuvunja vioo vya magari ya kubebea taka aina FAW SM 8726, na kuiba betri mbili za gari hilo na gari dogo aina ya Nissan lenye namba SM 2858 mali ya mamlaka hiyo.
Kulingana na tukio hilo vibaka wameweza kuonekana wakipora mali katika ofisi hizo huku wengine wakivunja chumba cha kuhifadhia mizigo mbalimbali na kufanikiwa kuiba mabati na viti na mali nyingi zilizokuwa zikibebwa,huku baadhi yao walionekana wamebeba madumu ya mafuta ya petroli wakitishia kuchoma jengo hilo.
Wanacnhi wa mjini hapa wanakumbuka matukio mbalimbali yanayojitokeza katika mji huu kuwa huwa yana leta adhari, kama ilivyo tokea katika matukio machache ya Februari 18, 2005 kufuatia wamachinga watano waliokamatwa Nakonde Zambia na mnao Septemba mosi hadi 3 mtu mmoja aliyefia katika mahabusu ya Nakonde nchini Zambia.
Mji wa Tunduma umekuwa kinala cha matukio ya vurugu na uvunjifu wa amani linapotokea jambo lolote hali ambayo huchangiwa na watu wanaojiita wana harakati kuongoza vikundi vya watu ambao huaribu na kupora mali za watu.
Mkurugenzi wa mji huu Aidan Mwanshiga alipotakiwa kuelezea uharibifu hu alisema kuwa tadhimini ya uharibifu uliotokea inafanywa na taarifa rasmi itatolewa.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya Diwani Athumani akizungumzia tukio hilo alisema kuwa tukio hilo haliwezi kuvumiliwa kutokana na kuwa maandamano ya wanafunzi hayawezi kupelekea kuvunjwa kwa ofisi za serikali bali kuna watu ambao wametumia mwanya huo ili kupora mali.
Aidha Kamanda Diwani alisema mbali ya uharibifu wa mali za Mamlika ya mji wa Tunduma hakuna madhala mengine yaliyotokea ikiwa ni pamoja na majeruhi au vifo vilivyojitokeza.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Momba Bwana Abiud Saideya amesema amesikitishwa sana na kitendo cha uharibifu wa nyaraka na mali za serikali na kudai kuwa hizo ni mali za wananchi,hivyo atahakikisha wale wote waliohusika na tukio hili wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Diwani wa Kata ya Tunduma Frank Mwakajoka amesema leo kutakuwa na mkutano wa hadhara wa kuzungumzia vitendo vilivyofanywa na watu hao ambao wamesababisha hasara kubwa kwa halmashauri.
Wakati huo huo katika Kata ya Vwawa wanafunzi wa shule za Ichenjezya na Haloli waliandamana hadi ofisi za halmashauri ya wilaya ya Mbozi na baada ya maandamano hayo walirejea shuleni kwao kwa amani huku wakisindikizwa na Polisi.
Wanafunzi hao walidai kuwa walimu wao walifika shuleni lakini hawakuwa tayari kufundisha wakiwaambia kuwa hawatafundisha kwa vile wapo kwenye mgomo hivyo waliwashauri waandamane hadi ofisi za halmashauri kudai haki yao hiyo.
Vilevile habari kutoaka Jijini Mbeya zimeeleza Mbeya zimeeleza kuwa mgomo ulianza mapema jana asubuhi, ambapo walimu walifika shuleni na kusaini kitabu cha mahudhurio kisha kukaa kimya huku wakiawaacha wanafunzi wakilandalanda bila cha kufanya.
Na: Ezekiel Kamanga,Tunduma
No comments:
Post a Comment